Watu wengine kamwe hawataweza kukusifu au kukubali kwa unachokifanya mpaka pale usipokuwepo kabisa. Ni ajabu kuwa watu wengine katu hawawezi kuona kile walichonacho; wakionacho pekee ni kile wasichonacho, ni kile wanachokosa.
Wakati mwingine inahitaji roho ya paka kuendelea na nguvu kufanya kile unachofanya wakati watu wanaendelea kukudhihaki.
Zaidi ya muziki, kuna kitu gani kizuri kinachoitangaza Tanzania nje ya nchi kwa sasa? Tusaidiane kuuchambua ukweli huu unaomezeka kwa fundo la mate la kulazimisha kinywani. Ni lini mara ya mwisho Tanzania imefanya vizuri kimataifa kwenye soka? Hakuna habari njema zaidi ya kuendelea kuwa kichwa cha mwendawazimu, iwe kwetu hata nje. Ni lini mara ya mwisho mkimbiaji riadha wa Tanzania ameshinda mbio zozote za kimataifa? Hakuna.
Kimichezo ni kama bado tumeendelea kuwa wasindikizaji tu. Au umesahau jinsi Selemani Kidunda alivyodundwa mwaka 2012 kwenye mashindano ya Olimpiki? Ukitoa mwaka 2005 pale Nancy Sumari alipokuwa Miss World Afrika, ni lini mrembo yeyote wa Tanzania amewahi kuiletea sifa nchi yetu?
Diamond akipata dhamana ya kuipaisha bendera ya taifa.
Ni nini hasa kinachoweza kuifanya Tanzania kuipeperusha bendera yake kwenye jukwaa la kimataifa kwa sifa nzuri? Au labda kipindi hiki tumegeuka kuwa mabingwa wa biashara ya dawa za kulevya na Watanzania ndio wamekuwa vinara wa kukamatwa kila kukicha nchi za nje.
Angekuwepo Kanumba na zile jitihada alizokuwa akizifanya, labda tungesema Bongo Movies ilikuwa inaelekea kuwa njia nzuri ya kutupa heshima pia. Lakini tangu afariki, hakuna mwingine anayeonesha dalili za kufanya kile alichokuwa anakifanya na filamu zetu zimeendelea kuwa za nyumbani pekee.
Hivyo, ukiangalia kwa mifano hiyo, ni muziki pekee wenye matumaini ya kuliongezea ‘k iki’ jina la nchi yetu kwenye ‘google search’. Lakini kama muziki ndio unaonekana kuwa kitu muhimu kinachoitangaza Tanzania, mbona wale wanaofanya vizuri kwa kutuwakilisha nje tunawabeza?
Mpaka muda huu, ukimtoa AY, hakuna msanii mwingine wa Tanzania anayevuma kimataifa kama alivyo Diamond Platnumz. Amefanikiwa kiasi cha hivi karibuni kumshirikisha staa wa Nigeria Davido kwenye remix ya wimbo wake, Number 1 na video iliyogharimu si chini ya dola 25,000. Amekuwa ni msanii mwenye kujituma, kutake risk na kutochoka kujaribu kufanya kile wengi wamekuwa wakikiogopa kufanya. Lakini bado kuna watu wengi hawaoni anachokifanya na wameendelea kumkejeli.
Wanasema hakuna binadamu aliye mkamilifu, lakini pamoja na kwamba unaweza kumnyonga mnyonge, ni vyema kukumbuka kumpa haki yake. Ni asili ya mwanadamu kuumizwa na mafanikio ya mtu mwingine, na ndio kinachotokea kwa Diamond. Ameendelea kufanikiwa kiasi mpaka anaanza kuwakera wengine. Si kosa kuchukia maisha na scandal zake, lakini si kosa pia kusifia kile anachoifanyia Tanzania.
Siwezi kubisha kuwa, mimi binafsi Diamond amekuwa akinikera kwa baadhi ya vitu (kama mimi pia ninavyokera wakati mwingine, nobody is perfect) lakini siwezi kuukataa ukweli kwamba Diamond ana kipaji, anajituma, anapendwa na anajua anachokifanya. Kubwa zaidi ya hayo, Diamond amekuwa mstari wa mbele kuitangaza Tanzania na Kiswahili pia lugha yetu adhimu kupitia nyimbo yake.
Ni jambo tunalolihitaji Watanzania kuwa na msanii wetu mkubwa mwenye hadhi na mafanikio kama ya P-Square. Pengine tusisahau ukweli huu kwamba ni mapenzi watakayoyapata wasanii wetu hapa nyumbani pekee ndio yatakayowapata mafanikio zaidi. Utafanikiwa vipi nje ya nchi kama nyumbani wanahate?
P-Square walikiri kuwa ni Wanaijeria wenyewe ndio waliowafanya wawe wakubwa kiasi hicho na kuwataka Watanzania pia wafanye hivyo kwa wasanii wao.
“Wanamuziki wenu wanafanya kile kile sisi tunachokifanya, mnaowaona watu hawa hapa?Mnaweza kuwafanya wawe wakubwa kuliko P-Square. Ukweli ni kwamba tunapromote muziki wa Africa. Waafrika huu ni muda wetu. Wamarekani nasema wanaogopa sasa hivi. Ningependa kuona mnaweka jitihada zaidi kwa wanamuziki wenu hapa. Nataka kuwaona wanakuja Nigeria na kuongoza concert. Hakuna mtu anayeza kufanya hivyo vizuri isipokuwa ninyi,” alisema Peter kwenye mkutano na waandishi wa habari jijini Dar, siku moja kabla ya show yao ya Leaders Club.
Diamond ni binadamu kama wengine. Anaumia anapoona anakosolewa hata katika mambo yasiyokuwa ya msingi. Kwa mfano hivi karibuni alihudhuria harusi ya Peter wa P-Square jijini Lagos, Nigeria. Inasemekana kuwa mwaliko huo aliupata kutokana na kuwa karibu na Iyanya aliyemshirikisha kwenye wimbo wake. Katika harusi hiyo, Diamond alipiga picha na Peter na kuiweka Instagram.
Diamond akiwa na Peter Okoye
Inasemekana kuwa P-Square walipokuja Tanzania waliulizwa kama wanamfahamu Diamond na kwamba wakasema lahashaa, hawamjui. Cha ajabu suala hilo limegeuka gumzo na watu wamekuwa wakimkejeli Diamond kuwa kaumbuka. Jamani, kwani ni lazima Peter awe anamfahamu Diamond? Amfahamu kwa njia ipi? P-Square ni wasanii namba moja Afrika, unaweza kufikiria ni wasanii wangapi Afrika wenye level za Diamond wanaotaka walau kupata contacts zao? Ni wengi mno, na unadhani ni rahisi kuwapata? Na hata hivyo, wote tunajua harusi zinavyokuwa na pilikapilika, unahisi Peter alikuwa na uwezo wa kumkariri kila mtu aliyehudhuria harusi yake. Unadhani ilikuwa rahisi kwa Diamond kujitambulisha vizuri kwa Peter kiasi cha kumfanya amkumbuke? Ni ngumu.
Haya, Rais Jakaya Kikwete alisema kwenye semina ya fursa kuwa Diamond ni msanii mwenye nidhamu ya kazi ama kwa Kiingereza ni ‘work ethic’. Wengi wemepingana na kauli ya mkuu wa nchi kwa kuona kampa Diamond sifa asiyostahili.
Lakini kwanza tujiulize, ni nini maana na nidhamu ya kazi? Ni thamani iendanayo na uchapakazi, umakini na kujituma. Nidhamu ya kazi ni pamoja na kuwa ‘reliable’ kuwa na uwezo wa kuanzisha vitu na kutafuta ujuzi mpya. Kwa tafsiri hiyo, unaweza kumpiga Rais Kikwete kwa kusema Diamond ana nidhamu ya kazi? Maisha binafsi, scandal na ubinadamu, havina uhusiano wowote na nidhamu ya kazi.
Lakini kwanza tujiulize, ni nini maana na nidhamu ya kazi? Ni thamani iendanayo na uchapakazi, umakini na kujituma. Nidhamu ya kazi ni pamoja na kuwa ‘reliable’ kuwa na uwezo wa kuanzisha vitu na kutafuta ujuzi mpya. Kwa tafsiri hiyo, unaweza kumpiga Rais Kikwete kwa kusema Diamond ana nidhamu ya kazi? Maisha binafsi, scandal na ubinadamu, havina uhusiano wowote na nidhamu ya kazi.
Sibishi kuwa wakati mwingine maisha ya Diamond hasa ya kimapenzi yamekuwa na sifa mbaya, lakini hiyo haiuondoi ukweli kuwa, ni msanii anayejituma sana. Tumkosoe pale ambapo anastahili kukosolewa na pia tumpe sifa pale anapostahili kusifiwa lakini sio kuhate pasipo na sababu za msingi.
Labda wengine wanamchukia kwasababu hupenda ‘kubrag’ kwa kupost picha za dola, cheni, saa, nguo ama viatu vya thamani kwenye Instagram? Kama ndivyo, basi nakumbuka kauli ya Joh Makini aliyosema hivi karibuni kuwa watu wengine wamekuwa na chuki kwa wenzao waliofanikiwa kwakuwa maisha kwao ni magumu.
“Ukichungunza kitu gani kinachosababisha haya mambo yote, utagundua kuwa watu wengi hawawezi kukidhi gharama za maisha jinsi ambavyo zinapanda. Huo ni mwanzo wa kuwekeana chuki kwenye kazi au mtu anakuwa anakuchukia wewe kwa kitu ambacho unafanya, utagundua ni kwamba kwasababu yeye anashindwa kulipia bili zake za kila siku, hata kama hausikika kwa namna moja au nyingine kwenye kipato chake lakini unakuta tu mtu anakuwa na chuki binafsi. Tatizo bei ya mkaa,” alisema Joh.
Ina make sense hata hivyo. Unapogundua kuwa huduma ya maji imekatwa nyumbani na huna hela ya kulipa au mchana unapita mkavu bila ‘kupiga menu’ halafu kwenye Instagram unaona picha ya Diamond akiwa na buruguntu la dola za kimarekani, lazima kiroho kiume na unajikuta unageuka hater ghafla!!!
Tuache chuki kwa wasanii wetu na tuwape nguvu kubwa ili waweze kuifikisha salama nchi yetu kimuziki.
No comments:
Post a Comment